Friday, August 17, 2012

KUMALIZIKA KWA MKUTANO WA JUMUIA YA USHIRIKIANO WA KIISLAMU (OIC) MJINI MAKKAH



Kilele cha mkutano wa dharura wa Jumuia ya Ushrikiano wa Kiislamu (OIC) kimefikia tamati yake mjini Makka kwa kusisitiza juu ya kulinda umoja wa Waislamu na kusimama imara dhidi ya “fitna” katika nchi za Kiislamu. Pamoja na hayo, mkutano huo ulikuwa na maazimio yafuatayo:
1.       Mkutano mkuu umetaka kusimamishwa haraka matumizi ya nguvu nchini siria pamoja na kulipeleka mbele ya umoja wa Mataifa suala la Waislamu wachache wa BURMA (MYANMAR) wanaonyanyasika na kukandamizwa.

2.       Wamelipokea na kulikubali pendekezo la mfalme Abdullah ibn Abdulaziz wa Saudi Arabia la kuanzisha kituo maalumu kwa ajili ya mazungumzo na maelewano baina ya Madhehebu za Kiislamu, kitakachokuwa na makao makuu mjini Riayadh, Saudia.

3.       Viongozi wa  nchi za Jumuia hiyo yenye wanachama 57 ambao wanawakilisha zaidi ya watu bilioni 1.5 duniani,  wamekubaliana juu ya “umuhimu na ulazima wa kulinda umoja wa nchi ya Syria na ardhi zake na kusimamisha mara moja matumizi yote ya nguvu pamoja na kusitisha uanachama wa Syria katika Jumuia ya Ushirikiano wa Kiislamu.”

4.       “Azimio la Makkah” limetaka “baadhi yetu kujitenga dhidi ya kutumia misimamo ya kimakundi na kimadhehebu katika kutumikia siasa na malengo yake badala ya kutumia siasa kwa ajili ya kuitumikia dini.”

5.       Tamko la azimio hilo limesisitiza “kusimama safu moja pamoja na jamii za Kiislamu zinazonyanyaswa na kuonewa mbele ya macho na masikio ya walimwengu wote na kukabiliana  na uadui wa kutisha unaofanywa dhidi ya wananchi wasiokuwa na msaada, wanaouawa na kuteswa.”

6.       Vilevile azimio hilo limesisitiza juu ya kusonga mbele katika “mapambano dhidi ya ugaidi na fikra potofu zinazosababisha suala hilo, kuulinda umma dhidi ya hilo janga na kutoyaruhusu makundi yanayochafua historia ya umma huu pamoja na kitabu chake na sunna za Mtume Wake.”

7.       “Kusimama safu moja katika kupambana na fitna ambazo zimeanza kupenya ndani ya kiwiliwili     cha Uislamu kwa misingi ya ubaguzi, madhehebu na makundi. Suala hilo litawezekana kwa kuheshimu utukufu na uhuru wetu na kutoingilia masuala ya ndani kwa kigezo cha nchi moja kuisimamia nchi nyingine na kwa kisingizio cha aina yoyote ile.”

8.       Vile vile azimio limetoa jukumu zito kwa vyombo vya habari katika “kuondosha fitna na kuimarisha misingi na malengo ya ushirikiano na mshikamano wa Kiislamu.”

9.       Pamoja na hayo, viongozi hao wa nchi za Kiislamu walitilia mkazo juu ya “umuhimu wa kadhia ya Palestina kwa kuizingatia kadhia hiyo kuwa ni mhimili wa umma wa Kiislamu na kukomesha ukaliaji wa mabavu wa Israel kwenye ardhi za Waarabu na Palestina tangu mwaka 1967 ikiwemo msikiti mtukufu wa Quds. Waliubebesha utawala vamizi wa Israel lawama ya kukwama kwa mazungumzo ya pande husika.

10.   Kwa upande mwingine, viongozi hao wa nchi za Kiislamu wameazimia kulipeleka suala la Waislamu wa Burma mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, huku wakikosoa vikali matumizi ya nguvu yaliyofanywa na watawala dhidi ya Waislamu hao.
Katika azimio la mwisho la Jumuia ya Ushirikiano wa Kiislamu, viongozi hao walielezea “masikitiko yao makubwa kwa utawala wa Myanmar (Burma) kutumia nguvu dhidi yao na kuwanyima haki ya uraia.”

Katibu Mkuu wa Jumuia ya Ushirikiano wa Kiislamu, Ekmeliddin Ihsanoglu  katika mkutano wake na waandaishi wa habari baada ya kikao cha mwisho cha Mkutano huo, alisisitiza kuwa viongozi wote wa Jumuia, katika mazungumzo yao, walijikita sana katika kadhia ya Waislamu wa Myanmar (Burma),  jambo linaloisisitizia Jumuia ya Kimataifa na Serikali ya Burma kwamba “zaidi ya Waislamu bilioni moja na nusu wamesimama nyuma ya Waislamu wa Burma.”

Mkutano huo ulikosoa vikali kile ulichokiita “uhalifu wa kibinaadamu” unaofanywa na Serikali ya Myanmar dhidi ya Waslamu wa chache wa nchi hiyo.
“Azimio la Makka” lilisisitiza kuwa “siasa za manyanyaso na matumizi ya nguvu zinazofanywa na serikali ya Myanmar dhidi ya raia wake Waislamu ni uhalifu dhidi ya ubinaadamu na ni jambo linalotakiwa kukosolewa na kupingwa vikali na mataifa yote ya ulimwengu wa Kiislamu kwa namna ya kipekee na mataifa ya ulimwengu mzima kwa ujumla.”
Viongozi hao wa nchi za Kiislamu wameitaka “Serikali ya Myanmar kuacha haraka vitendo hivyo na kuwapa Warohingya haki zao kama raia katika nchi ya Myanmar.”
Mkutano huo ulioitishwa na mfalme wa Saudi Arabia, ulihudhuriwa na marais wa nchi wapatao 40. 

No comments:

Post a Comment