Tuesday, August 21, 2012

KUMBUKUMBU YA 43 YA KUCHOMWA KWA MSIKITI WA AL-AQSASiku ya leo ya Jumanne inasadifiana na kumbukumbu ya 43 ya msiba mkubwa uliowakumba Waislamu kwa kuchomwa msikiti mtukufu wa Al-Aqsa, qiblah cha kwanza cha Waislamu na mmoja wa Misikiti mitatu mtukufu zaidi kwa Waislamu. Katika siku kama ya leo, Waislamu hukumbuka jinai mbaya iliyofanywa dhidi ya Msikiti huo Mtukufu na moto uliowashwa na mikono ya chuki na uadui.

Jinai hii iliamsha moto wa upinzani na hasira kubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Siku ya pili baada ya tukio hilo, maelfu ya Waislamu waliswali swala ya Ijumaa katika viwanja vya nje vya Msikiti huo Mtukufu, na baada ya hapo maandamano yakaenea mji mzima wa Qudsi kupinga kitendo hicho, jambo lililopelekea kufanyika mkutano wa kwanza wa nchi za Kiislamu mjini Rabat, Morocco.

 Aidha, tukio hilo ovu lilizusha radiamali (reaction) za kiulimwengu na kimataifa zikilipinga kwa nguvu. Hiyo ikapelekea Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutoa azimio lake namba 271, ambalo liliwatia hatiani wavamizi kwa kuuvunjia heshima msikiti huo na kuzitaka mamlaka vamizi za Israel kufuta hatua zote zitakazoathiri hali ya Mji huo Mtakatifu.

Azimio hilo lilielezea masikitiko ya Baraza hilo juu ya uharibifu uliosababishwa na moto huo kwenye Msikiti chini ya uvamizi wa Israel na kuitaka iheshimu mkataba wa Geneva na sheria ya kimataifa inayosimamia uvamizi wa kijeshi, na kuacha kukwamisha kazi ya Baraza la Kiislamu unaolenga kulinda, kuratibu na kuboresha maeneo Matakatifu ya Kiislamu.

Maadhimisho ya mwaka huu ya kuchomwa kwa msikiti Mtukufu wa Al-Aqsa yanakuja huku vita kali ikipamba moto dhidi ya Mji wa Qudsi (Jerusalem) kwa ujumla, na hasa msikiti wa Al-Aqsa, baada ya wazo hatari la Israel linalopendekeza kuigawa Al-Aqsa katika sehemu mbili za Waislamu na Wayahudi, pendekezo ambalo litakuwa na athari na matokeo mabaya sana kwa mustakbali wa Msikiti huo.

Vilevile, kumbukumbu za mwaka huu zinaweka mkazo kuwa mji wa Qudsi (Jerusalem) na maeneo yake matakatifu vitabaki kuwa mali ya Waislamu kwa namna yoyote ile, hata kama Utawala vamizi wa Israel utafanya nini katika kujaribu kubadilisha alama za mji huo Mtukufu na kujenga maelfu ya makazi ya walowezi wa Kiyahudi katika mji huo. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilisisitiza katika azimio lake lililotoka katika mwezi wa Juni, mwaka 1980 kwamba kuzikalia kwa mabavu ardhi hizo ni jambo lisilokubalika, huku Baraza hilo likisisitiza upinzani wake dhidi ya matendo ya kiuadui yanayofanywa na walowezi katika mji huo. Mwaka huohuo, Baraza lilizitaka nchi zenye balozi katika mji huo kuzihamisha.

Katika azimio la mwezi Juni, mwaka 1998, kwa mara ya kwanza, wanachama wote wa Baraza walikubaliana kuuzuia Utawala wa Kizayuni kujitanua katika mji huo na kuonesha kuwa kufanya hivyo ni kukiuka maazimio ya sheria za kimataifa.

No comments:

Post a Comment