Friday, March 23, 2012

Muujiza Wa Mbu -1

Kazi nyingi zinazofanywa na wanyama na matendo yao vinahitaji kiwango cha utambuzi, uzoefu, maarifa na utaalamu unaokwenda mbali zaidi ya kile wanachokifanya kwa kutumia kiwango cha akili walichonacho. Uchunguzi mdogo tu unatutosha kabisa kujua kwamba sio wanyama kama wao wanaotoa sifa hizo bora.

Fikiria uwezo wa ndege wanaohama maelfu ya kilomita wakiwa angani bila kuchoka,  usanifu wenye ujuzi wa ajabu unaotumiwa na buibui wakati kutengeneza mtandao wa nyuzi zake,  ushirikiano kamili na ugawanaji wa majukumu katika makoloni na himaya za wadudu chungu, jiometri ya ajabu ya katika masega ya asali yaliyojengwa kwa ushirikiano na maelfu ya nyuki, na mifano mingine mingi isiyohisabika...

Chanzo cha akili na utashi huu unaowawezesha wanyama ya kufanya mambo haya hakipatikani ndani ya  miili yao wala katika maumbile yao, bali kinapatikana katika uingiliaji kati wa ajabu wa akili na nguvu isiyoonekana ambayo hujidhihirisha katika kila hatua. Hata kama mmiliki wa akili na nguvu hii haonekani, uingiliaji kati huu katika matukio mbalimbali hutoa ushahidi wa kutosha wa kuwepo kwa nguvu hii ili kuondoa mashaka yote.

Wanasayansi wenye kufuata nadharia ya mgeuko (evolitionists) ambao walifahamu hili pia wanakubali kuwepo kwa nguvu iliyo nje ya uwezo wa viumbe hivyo kufanya kazi zao, lakini wanayawekea mpaka maelezo yao kuhusu mada hii kwa kuiita nguvu hii "silika." Kwa kuwa hawataki kumtambua mmiliki halisi wa nguvu hii wanaiita silika, vile vile wanaizulia jina na kuiita "maumbile mama." Hata hivyo, hadi sasa, hakuna mfuasi wa nadharia ya mgeuko ambaye ameweza kuonyesha kuwa hicho wanachokiita silika kinapata amri na maelekezo kutoka wapi, kukielezea kile wanachokiita "maumbile mama", kueleza iwapo kama ni jiwe, mti, mto, mlima, bahari au nyota.

Matokeo yake, wafuasi wa nadharia hiyo wamemtengeneza mungu wa kufikirika kutokana na kile wanachokiita "maumbile mama" na kutumia neno "silika" kwenye tabia inayotokana na amri na maongozo ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anasema ndani ya Qur’an Tukufu:

“Hamuabudu badala yake ila majina tu mliyo yapanga nyinyi na baba zenu. Mwenyezi Mungu hakuyateremshia hayo uthibitisho wowote...”
 

Qur’an Surat Yusuf 12: 40

Hivyo, kwa kuukataa ukweli wa mambo, wanajidanganya na kujaribu kuzifurahisha na kuzituliza dhamiri zao. Wanahisi kwa uwazi kabisa uwepo wa Mungu na sifa zake katika dhamiri zao, lakini wanaukimbia  "ukweli" na kuukana ushuhuda wa Mwenyezi Mungu. Sababu ya suala hili imeelezwa ndani ya Qur’an kama ifuatavyo:

“Basi zilipo wafikia Ishara zetu hizo zenye kuonyesha, wakasema: Huu ni uchawi dhaahiri. Na wakazikataa kwa dhulma na kujivuna, na hali ya kuwa nafsi zao zina yakini nazo. Basi angalia ulikuwaje mwisho wa mafisadi!” 

Qur’an Surat An-Naml 27: 13-14

Mwenyezi Mungu Mtukufu umeutandaza ushahidi wa uwepo Wake mbele ya macho ya mwanadamu. Akaufanya ujuzi Wake wa milele ujidhihirishe ndani ya viumbe wake wateule. Kwa fadhila zake zisizokuwa na kikomo, amewapa kazi kubwa viumbe wasiotarajiwa, dhaifu kabisa na hata wasiokuwa na ubongo. Matokeo yake, viumbe wengi, wakubwa kwa wadogo, kuanzia ndege mpaka nyoka, nyangumi mpaka wadudu, huonyesha tabia na matendo yasiyotarajiwa ambayo hujaza mshangao watu wengi. Tabia na mienendo hiyo huwastaajabisha mno watu wengi. Hata mwanadamu, ambaye anajiona kuwa kiumbe mwenye akili, ujuzi na utambuzi, amekuwa dhalili mbele ya ujuzi na ustadi mwingi wa viumbe hawa ( kwa mfano, uwezo wa buibui wa kuzalisha nyuzi imara zaidi ya chuma), na hana hata uwezo wa kumuiga.

Maudhui ya mada yangu hii,yaani mbu, ni mojawapo tu ya viumbe hao, ambaye vipengele vya tabia na mwenendo wake utatujaza mshangao. Na ingawa yeye ni kiumbe ambaye tumezoea kumuona na kukutana naye sana, yumkini ni kiumbe ambaye hatumfikirii na humuona kuwa asiyekuwa na maana yoyote.

Hivyo, waweza kujiuliza, “Kama ni hivyo, kwa nini azungumziwe mbu?” Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema ndani ya Qur’an Tukufu:

“Hakika Mwenyezi Mungu haoni haya kutoa mfano hata wa mbu na ulio wa zaidi yake. Ama wale walio amini hujua ya kwamba hiyo ni haki iliyo toka kwa Mola wao Mlezi, lakini wale walio kufuru husema: Ni nini analo kusudia Mwenyezi Mungu kwa mfano huu? Kwa mfano huu huwapoteza wengi na huwaongoa wengi; lakini hawapotezi ila wale wapotovu.”
Qur’an Surat Al- Baqara 2: 26

Yampasa mwanadamu anayeutambua ukweli huu autafakari kwa dhati ushuhuda wa uumbaji wa Mwenyezi Mungu na amuogope na kumkhofu Yeye tu.

“...Hujui kwamba Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu? Hujui kwamba Mwenyezi Mungu ana ufalme wa mbingu na ardhi? Nanyi hamna mlinzi wala msaidizi isipo kuwa Mwenyezi Mungu.” 

Qur’an Surat Al- Baqara  2: 106-107

No comments:

Post a Comment