Friday, March 23, 2012

Sosholojia Ya Qur’an Tukufu 1: Jamii Ni Nini?

Assalamu Alaikum Wa Rahmatu Allah Wa Barakatuh

Ndugu zangu katika imani, kwa kuwa Uislamu ni mfumo kamili wa maisha, ambao hauna shaka ndani yake, nimeonelea kwa mara nyingine tena niwaletee mfulululizo wa mada ya elimu –jamii (sociology) kwa mtazamo wa Qur’an Tukufu na Uislamu kwa ujumla, asaa tukafaidika na kitabu hiki kitukufu. Ni muhimu niwaeleze kuwa Qur’an Tukufu ni kitabu cha ajabu sana, ambacho hakuna mfano wake. Na hili linaendelea kudhihiri kila siku kwa wale wanaoidurusu na kuitafiti kwa undani kabisa kwa lengo la kujifunza. Wengine huiona Qur’an kama kitabu cha kusoma ili mtu upate thawabu tu basi. La hasha, Qur’an yenyewe inajitambullisha vipi? Je inajitambulisha kuwa ni kitabu cha kuwekwa kwenye kabati na kuangukiwa na vumbi? Je Qur’an inajitambulisha vipi? Haya, yenyewe yasema hivi:
“Hili ni Tangazo liwafikie watu, liwaonye, na wapate kujua kuwa hakika Yeye ni Mungu Mmoja, na wapate kukumbuka wenye akili.” (Qur’an 14: 52)
Hivyo ndivyo inavyojitangaza. Sasa kwa kuwa tukiizungumzia Qur’an hatuwezi kuimaliza, ni vyema niishie hapo ili nipate kuendelea na mada hii adhimu ambayo nimekuwa nikiitafiti kwa muda mrefu ndani ya Qur’an Tukufu.
Na sasa tutajaribu kwanza kuingalia jamii (society).

Jamii inaundwa na makundi ya binadamu yanayoungwanishwa pamoja kwa njia ya mifumo, desturi, taratibu na sheria maalumu, na kuwa na uwepo wa pamoja wa kijamii. Maisha ya pamoja ni yale ambayo makundi ya watu huishi pamoja katika eneo maalumu, na kushirikia/kuchangia (share) hali ya hewa moja na vyakula hivo hivyo. Miti ya bustani pia 'huishi' pamoja na kushirikiana moja ya hali ya hewa na chakula cha aina moja. Kwa namna hiyo, kundi la swara nalo pia hupata malisho pamoja, na kuhama pamoja kutoka eneo moja kwenda eneo jingine. Lakini huwezi kusema kuwa miti na swara/paa wana maisha maisha ya kijamii, kwa sababu hawaundi jamii.

Maisha ya binadamu ni ya kijamii kwa maana kwamba kimsingi/kwa asili ni wenye kupenda kushirikiana na wengine (gregarious). Kwa upande mwingine mahitaji, manufaa, kutosheka, kazi na shughuli za binaadamu ni za kijamii kwa asili, na mfumo wa kijamii hauwezi kudumishwa isipokuwa kwa njia ya mgawanyo wa kazi, mgawanyo wa faida na ridhaa ya pamoja ya mahitaji yaliyo ndani ya seti fulani ya desturi na mifumo. Kwa upande mwingine, mawazo na fikra, mienendo na tabia maalumu huwatawala na kuwaongza binaadamu kwa ujumla na kuwapa hisia ya umoja na ushirikiano. Kwa maneno mengine, jamii inawakilisha kundi la binadamu, ambao, kwa kulazimishwa na mlolongo wa mahitaji na kwa kuathiriwa na imani, maadili na malengo, huunganishwa pamoja na kutumbukia katika bwawa la maisha ya pamoja .

Maslahi ya pamoja ya kijamii, na mahusiano ya pekee ya maisha ya binadamu huwaunganisha pamoja binadamu na kumpa kila mtu mmoja mmoja hisia ya umoja sawa na hisia wanayokuwa nayo kundi la watu wanaosafiri pamoja katika gari au ndege au mashua wote wakielekea eneo moja , na kushirikiana matumaini ya pamoja ya kufikia mwisho wa safari salama, wakishirikiana kwa kila hatari ianayojitokeza katika safari na pia hatima ya pamoja.

Angalia jinsi Mtume wa Uislamu (s.a.w) anavyoieleza falsafa ya `kuamrisha mema na kukataza maovu '(al-'amr bil wa ma'ruf nahy` al-Munkar) kwa kutoa mfano ufuatao:
“Kundi la watu limepanda katika meli ambayo inasafiri kwa amani na kukata mawimbi. Kila mmoja wao amekaa kwenye kiti alichowekewa. Mmoja wa wasafiri akadai kuwa kiti alichokikalia mali yake na hakuna anayekimili zaidi ya yeye, akaanza kuchimba shimo chini ya kiti chake na kifaa chenye ukali. Kama wasafiri wote hawatomzuia kwa haraka sio wao wenyewe tu watakaokuwa katika hatari ya kuzama bali pia hata huyo masikini anayechimba shimo atazama.”

No comments:

Post a Comment