Friday, March 23, 2012

Ugonjwa Wa Kichocho (Bilharzia)

Tatizo hili huwapata watu wengi hasa watoto wanaocheza katika madimbwi ya maji wakati wa mvua au wanapotumia maji ambayo yana vijidudu vya maradhi hayo. Vijidudu vya kichocho humuingia binadamu na kwenda kuishi katika kibofu cha mkojo au utumbo wake.

Kwa kawaida kimelea cha kike hutaga mayai ambayo hutoka kwa mtu mwenye ugonjwa huo na kuingia katika maji ikiwa mtu huyo atakojolea maji hayo au wakati wa haja kubwa. Mayai hayo huanguliwa na kutoa viluilui ambavyo hupenya kwa konokono wa majini. Viluilui hawa baada kutoka kwenye mwili wa konokono huweza kumuingia binadamu na kupenya katika ngozi na kwenda kutulia ktka mishipa ya ini ambapo hukomaa na baada ya hapo hutoka na kuingia katika mishipa ya kibofu cha mkojo na njia ya haja kubwa  katika utumbo mpana.

Mgonjwa asipotibiwa haraka hupata matatizo katika njia ya haja kubwa na kibofu cha mkojo na wakati mwingine mayai ya kichocho huingia katika uti wa mgongo au katika ubongo na kusababisha matatizo.

Dalili
Kupatwa na homa siku 30 baada ya kunywa maji yenye maambukizi
Kikohozi kikavu na kujihisi kuchoka.
Baadaye damu huanza kutoka kwenye mkojo na haja kubwa lakini hatua hii ni baada ya ugonjwa kukomaa.

Ushauri
Kichocho ni ugonjwa unaotibika haraka kwa dawa iwapo itabainika mapema.
Watoto wazuiwe kuogelea katika madimbwi au maji yaliyosimama.
Kunywa maji masafi na salama.
Wanaoish kando ya mito, maziwa na bahari wasikanyage maji hayo bila kuwa na viatu maalumu vya kuzuia maji kupenya na mabwawa yote ya kuogelea yawekwe dawa ya kuua vijidudu.

Makala Haya Yameandaliwa Na Dokta Abdulazizi Maliki
Simu:
+255 714 909 563
+255 763 986 499

No comments:

Post a Comment