Friday, March 23, 2012

Mambo 10 Yanayokufanya Uwe Mume Bora

1.         Vaa vizuri kwa ajili ya mkeo, uonekane nadhifu na mwenye kunukia vizuri. Kama ambavyo mume anapenda mke wake aonekane maridadi kwa ajili yake, naye pia anapenda mume wake avae vizuri kwa ajili yake. Kumbuka kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w) daima alikuwa akianza kupiga mswaki pindi anaporudi nyumbani na daima alikuwa akipenda harufu nzuri.

2.        Muite mkeo kwa majina mazuri. Mtukufu Mtume (s.a.w) alikuwa akiwaita wakeze kwa majina mazuri ambayo hata wao wenyewe walikuwa wakipenda kuyasikia. Muite mkeo kwa jina zuri analolipenda zaidi kulisikia, na epuka kutumia majina yatakayoumiza hisia zake.

3.         Usiamiliane na mkeo kama nzi. Mara zote katika maisha yetu ya kila siku huwa hatukumbuki kuwa kuna nzi mpaka pale wanapotuudhi. Angalia, mkeo hukufanyia mambo mengi mema kwa siku nzima ambayo huwa huyaangalii, ila pale anapokufanyia kosa kidogo unamtazama. Usiishi naye kwa namna hii; yatambue mambo mema yote anayokufanyia.

4.         Ukiona kosa kutoka kwa mkeo, jaribu kuwa mkimya na usiseme! Hivi ndivyo Mtukufu Mtume (s.a.w) alivyokuwa pale anapoona jambo lisilokuwa muafaka kutoka kwa wakeze. Ni njia ambayo ni wanaume wachache wa Kiislamu wameimudu.

5.         Onyesha tabasamu kwa mkeo pindi unapomuona na daima zidisha kumkumbatia. Kutabasamu ni sadaqah na mkeo naye anastahili hiyo sadaka kwa namna ya kipekee. Fikiria maisha yatakavyokuwa pale mkeo anapokuona unatabasamu kwa ajili yake! Kumbuka pia zile hadith zinazosema kuwa Mtukufu Mtume (s.a.w) alikuwa akimbusu mkewe kabla ya kwenda kuswali, hata kama akiwa amefunga.

6.        Mshukuru kwa kila analokufanyia. Kisha mshukuru tena na tena! Angalia, mkeo anakuandalia chakula, anasafisha nyumba na anafanya kazi nyingine nyingi mno. Wakati mwingine hata kumpongeza hufanyi! Usiwe hivyo, mshukuru na useme: “Ahsante mke wangu!”

7.         Muombe akuandikie mambo kumi uliyomfanyia na yakamfurahisha. Kisha mfanyie mambo hayo tena. Mara nyingi huwa ni vigumu kujua mambo yanayomfurahisha mkeo. Huna haja ya kubahatisha, muombe akwambie na kisha uyafanye hayo na mengine pia katika kipindi chote cha maisha yenu.

8.         Usiyapuuze na kuyabeza matakwa yake. Mfariji. Wakati mwingine wanaume huyadharau maombi ya wake zao. Mtukufu Mtume (s.a.w) hakuwa hivyo.

9.         Uwe mwenye kunyumbulika na fanya michezo na mkeo. Mtukufu Mtume (s.a.w) alikuwa akishindana na mkewe bibi Aisha katika mchezo wa kukimbia. Mara ya mwisho umemfanyia lini mkeo jambo kama hilo?

10.       Daima kumbuka maneno ya Mtukufu Mtume (s.a.w): “Mbora wenu ni yule anayeitendea mambo bora familia yake. Nami ni mbora wenu kwa familia yangu.” Jaribu kuwa bora!

Usisahau kumuomba Mwenyezi Mungu aifanye ndoa yako kuwa bora.

No comments:

Post a Comment